
Pumziko Katika Ulimwengu Wenye Wahaka
Muhtasari
Msongo wa mawazo na kufanyakazi kupita kiasi huwapeleka watu wengi kaburini kabla ya wakati wao. Lakini katika uumbaji, Mungu aliandaa tiba kwa ajili ya tatizo la msongo wa mawazo: siku ya pumziko. Siku hii takatifu iliwekwa kama baraka ili wanadamu waweze kupumzika baada ya kazi zao na kutumia muda wao na Mungu. Cha kusikitisha, ingawa Mungu aliwaagiza wanadamu kuikumbuka, wengi wameisahau hii siku maalumu, na wengi wamemsahau hata Muumba ambaye aliwapatia siku hiyo.
Aina
Kijitabu
Mchapishaji
Sharing Hope Publications
Inapatikana katika
38 Lugha
Kurasa
6
Mita Duran alikuwa amekufa. Binti Mwindonesia mwandishi mahiri wa matangazo ya biashara mwenye umri wa miaka 24 alianguka tu kutoka katika dawati lake. Nini kilikuwa kimetokea?
Mita alifanya kazi katika wakala wa matangazo, ambapo matarajio yalikuwa juu mno na mzigo wa kazi ulikuwa mzito. Kabla tu ya kifo chake, alieleza katika mitandao ya kijamii juu ya kuchoshwa kwake: “Jioni hii nimebeba funguo za ofisi kwa siku ya nane mfululizo. Sipati fursa ya kufurahia maisha.”
Alitegemea sana kinywaji chenye kafeini kiitwacho Krating Daeng, toleo la Asia la Red Bull. Maoni yake ya mwisho mtandaoni yalikuwa: “Saa 30 za kufanya kazi na bado najisikia mwenye nguvu.” Kisha binti huyu alianguka toka katika dawati lake na hakuweza kuamka tena.
Nini kilitokea? Mita alikufa kutokana na kufanyakazi kupita kiasi.
Leo, wengi wetu tuna ratiba za kazi zenye shughuli nyingi. Jamii inatuhimiza kufanyakazi zaidi, ili kupata kipato kikubwa zaidi na kuweza kununua vitu vingi zaidi. Tunasumbuliwa na msongo, kukosa usingizi na kuuchosha ubongo.
Yawezekana hatujiui kama Mita, lakini maisha yanaweza kuwa mzigo mzito. Je hiki ndicho Mungu alichokusudia kwa ajili yetu? Yeye Ndiye Mtoaji wa Amani. Tunapojitumikisha kupita kiasi, je tunajisikia kuwa na amani? La, hasha!
Ikiwa tumezidiwa na uchovu, ni lazima itakuwa kwamba tunasahau kitu fulani ambacho Mungu anataka tukikumbuke. Hebu tugundue kile ambacho amekisema juu ya pumziko.
Kubonyeza Kitufe cha “Pauzi”
Mungu ni Mwingi wa Neema na Mwingi wa Rehema. Alijua kwamba wanadamu wanahitaji muda wa kujaza upya nguvu zao za kimwili, kiakili na kiroho, kama ilivyo kwa simu za mkononi na kompyuta mpakato. Kwa hiyo nabii Musa aliandika amri ya Mungu:
Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana Mungu wako. Siku hiyo usifanye kazi yoyote (Kutoka katika sehemu ya kwanza ya Biblia, ambayo pia hujulikana kama Torati: Kutoka 20:8–10).
Amri hii isiyobadilika ya Mwenyezi Mungu inatuambia tuikumbuke siku ya saba. Kwa mujibu wa lugha nyingi za ulimwengu, siku hii ya saba iliyowekwa wakfu kwa ajili ya kupumzika inaitwa “Sabato.” Kwa nini Mungu alituamuru kuikumbuka? Kwa vile anajua kwamba kusahau kumekuwa ni tatizo linaloendelea katika jamii ya wanadamu, kuanzia kwa Adamu. Imetupasa kutosahau amri za Mungu, kwani ni pale tu tunapomkumbuka Yeye na amri Zake ndipo tutadumishwa kutembea katika njia nyofu.
Lakini kwa nini Sabato ni ya pekee? Mungu anatuambia,
Maana, kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba. Kwa hiyo Bwana akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa (Kutoka 20:11).
Sabato ni kumbusho muhimu kwamba Mungu ndiye Muumbaji. Watu wengine hutoa sababu ya kupinga kwamba kwa kuwa Mungu hachoki, asingehitaji kupumzika katika siku ya saba. Lakini Mungu hakupumzika kutokana na uchovu; Aliacha kazi Yake ya kuumba ili apate kutuwekea muda mtakatifu wa kupumzika.
Mungu aliona kwamba siku ya kupumzika ni ya manufaa kwa jamii ya wanadamu. Aliifanya siku ya saba kuwa Sabato, ikimaanisha kituo au pumziko. Hivyo, siku ya saba ya kila wiki ni siku maalum ya kubonyeza kitufe cha “pauzi.” Tunapaswa kupumzika kutokana na kazi na shughuli zisizo za kidini kwa siku nzima ili tupate kumkumbuka Yeye na kumwabudu.
Je lisingekuwa jambo la kufurahisha sana ikiwa bosi au profesa wako angekuamuru kutumia muda zaidi kupumzika? Na kwa kweli hiki ndicho hasa Mungu ameamuru! Mungu na asifiwe! Kwa kweli Yeye ni mwingi wa rehema!
Kuitakasa Siku ya Mungu
Sabato ni Siku takatifu mahali pote kwa ajili ya watu wote ulimwenguni. Ilishikwa na waamini Mungu mmoja wanaomwamini Mungu pekee wa kweli aliye Muumbaji muda mrefu kabla ya Wayahudi, Wakristo, Waislamu, Wabudha, au Wahindu kuwepo. Kwa kweli, ilikabidhiwa kwa jamii ya wanadamu wakati ulimwengu ulipoumbwa. Adamu na Eva (anayejulikana pia kama Hawa) waliishika Sabato, na kamwe Mungu hajawahi kutupatia idhini ya kusahau kile alichotuambia tukikumbuke.
Cha kusikitisha ni kwamba, mara nyingi Sabato imesahauliwa. Manabii waliwaonya Wayahudi wa kale kwamba Mungu angeleta maangamizo kwao ikiwa wangeisahau Sabato. Hawakuzingatia onyo hilo, hivyo Yerusalemu iliangamizwa, na familia zao zilipelekwa uhamishoni. Wakristo pia waliisahau Sabato kwa kubadili siku yao takatifu kwenda Jumapili kinyume na amri ya Mwenyezi Mungu. Waislamu huabudu katika siku ya Ijumaa lakini wamesahau kwamba ili tuishi kwa utii mkamilifu kwa Muumba imetupasa kupumzika katika siku ya saba.
Ni kwa nini inaonekana kana kwamba dunia yetu yote inaisahau siku hii ya muhimu? Je kuna sababu yoyote mbaya zaidi inayosababisha usahaulifu huu ulioenea sana?
Yesu Masihi alituonya juu ya mamlaka inayokuja ya ulimwengu wote ambayo Shetani (Sheitwani) ataitumia kugeuza akili zetu kutoka kwa Muumba wetu. Mamilioni watadanganyika na kuabudu katika sabato ya uongo. Kama Shetani akiweza kutufanya kuisahau siku ya Muumba, anaamini kuwa tutamsahau Muumba Mwenyewe. Hata hivyo, tunapoitunza Sabato ya kweli, tunaonesha utii wetu kwa Muumba wetu, na kunufaika na zawadi ya pumziko, utulivu, na amani.
Kuingia katika Pumziko la Mungu
Nabii Musa aliandika kwamba “Mungu akaibarikia siku ya saba” (Torati, Mwanzo 2:3). Je umechoka na kudhoofu? Kuna mibaraka katika Sabato!
Mita Duran, mwandishi wa matangazo kutoka Indonesia, alikufa kutokana na kufanya kazi kupita kiasi, lakini haipaswi kuwa hivyo kwako. Mungu anakualika upate kupumzika kwa kuacha kazi zako kila juma na kupata uzoefu wa mibaraka ya Sabato.
Kama ungependa kujifunza zaidi juu ya jinsi Mungu anavyotupatia pumziko, amani, na uponyaji, tafadhali wasiliana nasi kupitia katika taarifa iliyo nyuma ya karatasi hii.
Copyright @ 2023 by Sharing Hope Publications. Kazi hii yaweza kuchapishwa na kusambazwa kwa watu wengine bure pasipo kuomba idhini kwa makusudi yasiyo ya kibiashara.Swahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Jisajili kwa ajili ya jarida letu
Kuwa wa kwanza kujua pale machapisho mapya yanapotoka

Tafuta Hadhira Yako
Machapisho Yaliyoangaziwa
© 2023 Sharing Hope Publications