
Je unahitaji muujiza?
Muhtasari
Mungu ana historia ya muda mrefu ya kuwafanyia miujiza watu Wake wakati ambapo waliihitaji hasa. Biblia hutueleza visa vingi juu ya unabii uliotimia, watu walioponywa, na matukio ya ajabu sana ambayo yaliwezekana tu kama majibu ya maombi. Kitini hiki kinatupatia sababu kadhaa za kuwa na imani na Biblia kama neno la Mungu lisilobadilika na jinsi unavyoweza kumwendea Mungu ili upate muujiza wako.
Aina
Kijitabu
Mchapishaji
Sharing Hope Publications
Inapatikana katika
38 Lugha
Kurasa
6
Ukoo mmoja mkubwa sana wa wanafamilia ulikuwa ukitumainia kupata maisha bora na hivyo ukaamua kuhama kwenda katika nchi mpya. Safari, hata hivyo, haikuwa rahisi; ilibidi wavuke jangwa kubwa kwa miguu. Kulikuwa na nyoka, nge, na joto kali. Iwapo wale wanaukoo waliokuwa wagonjwa au dhaifu walibaki nyuma ya msafara, walishambuliwa na maharamia.
Mara wakaishiwa chakula, lakini kiongozi wao akamlilia Mungu awafanyie muujiza. Siku iliyofuata, watu walipoamka walikuta vipande vidogo vidogo sana vya kitu kilichoonekana kama mkate vimeenea kote juu ya ardhi. Vilikuwa vitamu kama biskuti nyembamba na asali. Na kulikuwako na kiasi cha kutosha kumshibisha kila mtu! Iliwachukua siku nyingi kulivuka jangwa lile, na kila siku aina hii ya mkate ilishuka kama mvua toka mbinguni. Bwana asifiwe, waliokolewa!
Kisa hiki chaweza kusikika kama cha kustaajabisha, lakini ni kweli kilitokea. Ni moja ya miujiza mingi inayosimuliwa katika Biblia, ambayo waweza kuijua kwa majina ya Torati, Zaburi, na Injili. Biblia ina mamia ya visa vya kweli, vingi vikiwa vimejengwa katika miujiza ambayo Mungu aliifanya katika maisha ya watu. Ni kitabu muhimu kwa nyakati zetu, ambapo watu wengi wanahitaji kufanyiwa miujiza.
Miujiza ya Kisasa
Katika miaka ya hivi karibuni, tumeshuhudia vita vya wenyewe kwa wenyewe, mapinduzi, kuporomoka kwa uchumi, kukosekana kwa ajira, magonjwa ya kuambukiza, na vifo. Mimi sina hakika hali yako ikoje kwa sasa. Yawezekana umelazimishwa kuhama toka nyumbani kwako. Yawezekana una mpendwa wako ambaye maisha yake yananing’inia kati ya kifo na uzima. Yawezekana unahangaika kutafuta kazi.
Haidhuru hali yako ikoje, Mungu anakujali na yuko tayari kukufanyia muujiza leo kama alivyokuwa nyakati za zamani. Unapojisikia kuwa na huzuni, unaweza kupata neno la kukutia shime kwa kusoma Biblia, kitabu cha miujiza.
Maneno ya Mungu kwa Ajili ya Wakati Wetu
Baadhi ya watu wanasita kusoma Biblia kwa sababu wamesikia kwamba kwa namna fulani imebadilishwa. Huenda uelewa huu mbaya ni kwa sababu ya mtindo wa maisha wa watu wengi wanaodai kuifuata Biblia. Nyakati zingine tunawaona Wakristo wakinywa pombe, wakicheza kamari, wakivalia isivyo staha, wakila nyama ya nguruwe, na wakiwanyanyasa watu.
Lakini kwa kweli, makosa yote haya yanakatazwa katika Biblia. Wakristo wanapoishi maisha yasiyo na utii kwa Mungu, hiyo haibadilishi uhalali wa Neno Lake la milele. Nabii Isaya aliandika, “Majani yakauka, ua lanyauka; Bali neno la Mungu wetu litasimama milele” (Isaya 40:8). Je unadhani wanadamu wana mamlaka ya kutosha kubadili Neno la Mungu, au inaelekea zaidi kwamba wanaliwakilisha vibaya kupitia kwa tabia zao mbaya?
Biblia hueleza juu ya wakati ambapo nabii Daudi (anayejulikana pia kama Daud) na watu wake walipokuwa wakisafirisha sanduku la agano, sanduku kubwa la dhahabu ambalo ndani yake kulikuwa na amri kumi. Amri Kumi zilikuwa ni sheria za Mungu za maisha ya kimaadili na zilikuwa zimeandikwa katika mabamba mawili ya mawe na kuwekwa katika sanduku la agano la dhahabu. Katika msafara ule mtu mmoja alidiriki kunyoosha mkono na kuligusa sanduku la agano-na mara ile alidondoka chini akafa!
Kama Mungu hakuruhusu mikono yenye kiburi kugusa sanduku takatifu ambalo lilikuwa na Neno Lake ndani yake, angewezaje kuruhusu watu waovu kulikaribia Neno Lake lililoandikwa wakiwa na mikasi na kalamu ya kufanyia marekebisho? Mungu ni Mkuu vya kutosha kulilinda Neno Lake.
Kwa kusema bila upendeleo, Biblia ndicho kitabu kilichohakikishwa kabisa katika historia ya mwanadamu. Muda si mrefu uliopita, wachungaji watatu Mabedui kule Palestina—Mohammed edh-Dhib, Juma Mohammed, na Khalil Musa—bila kutarajia waligundua Magombo ya Bahari ya Shamu. Huu ulikuwa ni uvumbuzi mkubwa wa kiakiolojia uliotupatia nafasi ya kulinganisha Biblia ya sasa na miswada ya kale ya Biblia ambayo ina umri wa karibu miaka 2000. Huo mlingano ni wa kustaajabisha, kwa mara nyingine tena ukionesha ukweli kwamba ufunuo wa Mungu hauwezi kubadilishwa. Kama unahitaji muujiza, unaweza kuwa na hakika kwamba Biblia ndiyo mahali pa kuaminika pa kuutafuta! Hapo utapata visa vya kustaajabisha vya manabii kama Nuhu, Ibrahimu, Yusufu, Yona, Danieli, Daudi, na Sulemani. Yawezekana umewahi kusikia vipande vya habari juu yao sehemu zingine, lakini Biblia inaeleza kisa chote!
Njoo Upate Muujiza Wako
Haidhuru unapitia zahama gani, Biblia ina kisa cha muujiza kwa ajili yako wewe:
Je wewe au mpendwa wako anasumbuliwa na ugonjwa? Soma juu ya uponyaji wa kustaajabisha wa Naamani, Jemadari wa jeshi la Shamu aliyekuwa na ukoma.
Je unapambana kupata chakula kwa ajili ya familia yako? Soma juu ya mjane wa Lebanoni na mwanawe, walionusurika katika njaa ya muda mrefu kwa kutegemea chupa ndogo tu ya mafuta na unga kidogo tu ambavyo kamwe havikuisha.
Je maisha yako yapo hatarini? Soma habari za Ebedmeleki, mtumwa Mkushi katika nyumba ya mfalme, ambaye maisha yake yaliokolewa wakati wa vita kwa sababu ya imani yake kwa Mungu.
Je unajisikia kama vile umetengwa na jamii? Soma habari za Hajiri Mmisri, ambaye aliona miujiza ya Mungu alipokuwa amekataliwa.
Je unazama chini ya shida za maisha? Soma juu ya wakati ule Yesu Kristo aliponyoosha mkono wake na kutuliza dhoroba kali na kuwaokoa wanafunzi wake kutoka katika uwezekano wa meli yao kuvunjika.
Majibu ya Kimuujiza
Tunapoisoma Biblia, tunajazwa na ujasiri wa kuomba kwa mioyo iliyojaa matarajio. Yesu Kristo alisema, “Na yo yote mtakayoyaomba katika sala mkiamini, mtapokea” (Mathayo 21:22). Tunaposoma visa vya watu wengine waliopokea miujiza toka kwa Bwana, mioyo yetu inavutiwa kwa matumaini kupeleka maombi yetu kuelekea mbinguni.
Je unahitaji muujiza? Hebu utiwe moyo na miujiza iliyomo kwenye Biblia na umwombe Mungu akufanyie ule ulio wako mwenyewe. Kwa hakika atasikia ombi lako leo!
Kama ungependa kujifunza zaidi juu ya miujiza katika Biblia, tafadhali wasiliana nasi kupitia katika taarifa iliyo nyuma ya karatasi hii.
Copyright @ 2023 by Sharing Hope Publications. Kazi hii yaweza kuchapishwa na kusambazwa kwa watu wengine bure pasipo kuomba idhini kwa makusudi yasiyo ya kibiashara.Swahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Jisajili kwa ajili ya jarida letu
Kuwa wa kwanza kujua pale machapisho mapya yanapotoka

Tafuta Hadhira Yako
Machapisho Yaliyoangaziwa
© 2023 Sharing Hope Publications