
Jinsi ya Kufikiri kwa Kujitegemea
Muhtasari
Manabii wa Mungu walitabiri juu ya mamlaka hatari ya kidini kwa jina la kiishara "Babeli." Kwa mujibu wa unabii, mamlaka hii itajaribu kutulazimisha na kutulaghai kuingia katika ibada ya uongo. Njia pekee itakayotuwezesha kupata usalama ni kufanya maamuzi yetu wenyewe na kudumisha utii usioyumba kwa neno la Mungu lililofunuliwa. Kitini hiki kinatueleza jinsi ya kutumia akili zetu ili tupate kuwa waumini wenye hekima wanaotumia akili zao katika nyakati za majanga ya ulimwengu mzima.
Aina
Kijitabu
Mchapishaji
Sharing Hope Publications
Inapatikana katika
38 Lugha
Kurasa
6
Ndo kwanza tulikuwa tumefika katika kilele cha Gunung Datuk baada ya kupanda kwa muda mrefu. Niliketi chini na rafiki yangu mpya, Adzak, kufurahia mandhari ile. Punde, mazungumzo yetu yaligeukia katika mada za kidini.
“Mimi ni mwanafikra huru” alidai Adzak. “Nina mtazamo wangu binafsi juu ya ulimwengu.”
“Ndio,” nilijibu. “Nimewasikia vijana wengi wa Malaysia wakajitambulisha kama wanafikra huru.”
Adzak akacheka. “Inatupasa kujitegemea katika kufikiri. Vinginevyo kuna kuchanganyikiwa kwingi. Kutakutia wazimu.”
“Lakini vipi wewe unaporudi nyumbani?” Niliuliza. “Hapa Malaysia, vijana wengi wanajiita wanafikra huru, lakini nyumbani, unatarajiwa kushiriki katika kaida za Kiislamu au Kibudha. Unawaambia nini wazazi wako?”
“Siwaambii,” alijibu Adzak. “Ninafuata tu yale wanayotaka. Naweza kuwa na fikra huru, lakini ninalazimika kuzihifadhi moyoni.”
Je Kuwa na Fikra Huru ni Muhimu?
Katika baadhi ya sehemu za ulimwengu, kuwa na imani potofu kunaweza kukufanya utengwe na jamii yako, ufukuzwe kazi, au hata kuuawa. Kufikiri kwa ajili yako wewe mwenyewe kunaweza kuwa jambo la hatari. Lakini je, ni jambo muhimu?
Ulimwengu wetu umesheheni mawazo mabaya na mawazo mazuri. Namna moja muhimu ya kuanza kupembua mazuri kutoka katika mabaya ni kuyatafakari na kuyazungumza. Kama ukinunua kitu cha gharama kubwa—kama vile dhahabu, zafarani, au simu aina ya Aifoni—hutalipia tu na kuondoka nayo. Lazima uikague, na kuilinganisha na bidhaa za washindani wake ili ujiridhishe kuwa unanunua kitu cha ubora wa hali ya juu. Mawazo pia lazima yatendewe vivyo hivyo.
Kuna kuchanganyikiwa kwingi duniani, na hali inakuwa mbaya zaidi wakati watu wanapojaribu kushinikiza mawazo yao yaliyokanganyika kwa jamii. Hebu ngoja nikujulishe juu ya unabii wa muhimu. Katika kitabu cha zamani sana kiitwacho “Ufunuo wa Yesu Kristo,” unabii unaeleza juu ya watu wanaojaribu kushinikiza mawazo yao ya kidini yanayokanganya kwa watu wengine. Kinasema “Umeanguka, umeanguka Babeli, mji ule ulio mkubwa, maana ndio uliowanywesha mataifa yote mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake” (Ufunuo 14:8).
Maneno hayo ya kiishara si magumu kuelewa. Babeli ulikuwa mji maarufu wa kale, lakini jina lake lina maana ya “machafuko.” Mji huu, “umeanguka” si kwa sababu umechanganyikiwa bali ni kwa sababu hautaki kuachana na kuchanganyikiwa kwake. Unashawishi mataifa kujiunga na uasherati wake wa kiroho—yaani kumsaliti Mungu kwa kuchanganya ibada ya ukweli na uongo. Haya mawazo ya uongo yanafanywa kuwa ya kawaida na kukubaliwa. Unabii huu juu ya “Babeli” unataja chombo cha kiroho cha ulimwengu mzima ambacho si tu kwamba kinayafanya kuwa ya kawaida makosa ya kiroho bali hatimaye kitathubutu kuyashinikiza kwa watu wanaoshikilia ukweli.
Ufunuo wa Yesu Kristo ulitabiri kwamba hilo lingetokea katika siku zetu. Huenda tayari umeliona hili likitokea. Je kuna watu wanaomwakilisha Mungu kwa mawazo potofu? Je umewahi kujisikia kuwa na wasiwasi sana katika dhamiri yako?
Ndio, hii ndiyo sababu kufikiri kwa uhuru ni muhimu.
Jinsi ya Kufikiri kwa Ajili Yako Mwenyewe
Watu wengi wanaridhika kufuata dini ya jamii yao. Hawazitafakari imani zao. Wanafuata mapokeo ya kidini ambayo hayana mantiki au ambayo yana madhara makubwa zaidi. Nyakati zingine hata viongozi wa kidini, ambao wanapaswa kutuonesha njia ya kwenda kwa Mungu, wao wenyewe wamejawa na upotofu.
Tutaupataje ukweli? Napendekeza kwamba tuwaamini manabii. Kwa nini? Kuna sababu tatu:
Manabii wanaonesha maarifa ya kustaajabisha ya siku za usoni. Nabii Danieli alitabiri juu ya kuinuka kwa Ulaya hadi kufikia nafasi yake ya kihistoria ya kutia ukoloni ulimwenguni. Yesu Kristo (ambaye pia anaitwa Isa al-Masih) alitabiri juu ya kuangamizwa kwa Yerusalemu mwaka 70 B.K. Nabii Musa alitabiri juu ya historia ya Ishmaeli hadi mwisho wa wakati.
Manabii wanaonesha maarifa ya ajabu ya kisayansi juu ya afya. Nabii Musa aliyeishi takriban miaka 3,500 iliyopita, alielezea karantini, udhibiti wa maji taka kwa ajili ya kuleta afya na kanuni za kuondoa bakteria. Aliwagawanya wanyama kati ya waliosafi na walio najisi. Na alituambia tusile damu au mafuta tunapokula nyama safi. Hata leo wale wanaofuata kanuni zake za chakula na usafi wanaishi miaka 15 zaidi ya watu wengine kwa jumla.
Mungu hujibu maombi ya waumini wanaomtumainia na wanaowaamini manabii Wake.
Maandishi ya manabii yamejaa tele miongozo—lakini ili tupate kunufaika nayo, ni lazima tujifunze kufikiri kiumakinifu, kupima imani zetu, na kupima usahihi wa ushahidi wa imani yetu. Kufikiri ni sehemu muhimu ya dini ya kweli.
Sasa, nini kinatokea tunapolichunguza kosa? Mwanzoni laweza kuonekana kama kweli. Lakini kadiri tunavyotafuta ushahidi, tunaanza kuona shida za wazo hilo.
Ukweli ni kinyume kabisa. Haupotezi chochote unapochunguzwa kwa makini. Kadiri tunavyozidi kuuchunguza ndivyo tunavyozidi kuona ukweli.
Waumini wanapaswa kuwa watu wenye hekima kabisa ulimwenguni kwa vile Mungu anawaongoza katika njia ya hekima. Unapojikuta katika hali ambapo huruhusiwi kufikiri kwa uhuru, au kuuliza maswali, basi hiyo haitoki kwa Mungu. Anataka tufanye uchunguzi wa kina kwa sababu ukweli ni madhubuti kiasi cha kustahimili uchunguzi. Lakini Babeli hukushawishi kuingia katika uongo na kukushikilia humo kwa kufunga milango ya nguvu za akili.
Kama umechanganyikiwa kiasi kwamba unahisi kana kwamba uko Babeli, toka huko! Njoo katika njia ya Mungu ya hekima. Fikiria mwenyewe na uulize maswali ya msingi. Hutajuta.
Je ungependa kujua zaidi juu ya Ufunuo wa Yesu Kristo? Tafadhali wasiliana nasi kupitia taarifa iliyo nyuma ya karatasi hii.
Copyright @ 2023 by Sharing Hope Publications. Kazi hii yaweza kuchapishwa na kusambazwa kwa watu wengine bure pasipo kuomba idhini kwa makusudi yasiyo ya kibiashara.Swahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Jisajili kwa ajili ya jarida letu
Kuwa wa kwanza kujua pale machapisho mapya yanapotoka

Tafuta Hadhira Yako
Machapisho Yaliyoangaziwa
© 2023 Sharing Hope Publications