Shauku ya Kupata Rehema

Shauku ya Kupata Rehema

Muhtasari

Je, rehema za Mungu zikoje? Je, anasema tu, "nakusamehe," au je, anatoa kitu mbadala kusafisha kumbukumbu zetu za aibu? Kitini hiki kinaeleza kisa kinachoendana na mazingira yetu ya asili ili kusaidia kuelezea hitaji la na maana ya kafara mbadala. Wasomaji watapata tumaini kujua kuwa dhambi yao inaweza kusamehewa na aibu yao kuondolewa.

Aina

Kijitabu

Mchapishaji

Sharing Hope Publications

Inapatikana katika

38 Lugha

Kurasa

6

Pakua

Fatuma alikuwa amebaki peke yake katika sikukuu ya Id el-Adha, na upweke wake ulikuwa zaidi ya alivyoweza kustahimili. Upweke wake ulitokana na makosa yake mwenyewe, au siyo? 

Fatuma alikumbuka jinsi alivyokuwa amebishana vikali na baba yake kuhusu kuolewa na Ahmed. Alikuwa ni binti mdogo aliye katika mapenzi. Baba yake angewezaje kukataa? Alipotoroka na kwenda kuolewa na Ahmed, baba yake alisema kamwe asije akarejea nyumbani.

Alidhani kuwa angeweza kustahimili aibu kwa sababu ya upendo wake kwa Ahmed. Lakini punde, alilazimika kukiri kuwa baba yake alikuwa sahihi. Ahmed hakuwa mtu yule ambaye binti huyu alidhani alikuwa amependana naye. Alimtelekeza na kumchukua mwanamke mwingine.

Fatuma alijionea haya. Aliamini kuwa alikuwa akipokea malipo ya haki kwa ajili ya msimamo wake. Aliielewa haki vizuri. Lakini lo, ni jinsi gani moyo wake ulitamani kupata rehema!

Yeye aliye Mwingi wa Neema na Mwingi wa Rehema

Kusema kweli, sote tumefanya makosa na kuipuuzia sauti ya hekima. Tumewakosea watu wengine. Watu wengine wametukosea. Jumuia zetu zinaundwa na watu wanaofanya makosa. Na ni jinsi gani ilivyo vigumu kusameheana na kujisamehe! 

Je kuna rehema kwa ajili ya makosa yetu?

Tafakari ni mara ngapi umeikariri aya rahisi “bismillahi Al-Rahman Al-Rahim”—“Kwa jina la Mungu, Mwingi wa Rehema, na Mwingi wa Neema.” Kuna nini cha pekee sana kuhusiana na rehema?

Huenda ni kwa sababu jamii zetu—na mioyo yetu wenyewe—inahitaji mno rehema.

Rehema: Njia Iliyo Bora

Miaka kadhaa iliyopita, mtu mmoja aliyeitwa Abdul-Rahman alipigana na jirani yake aliyeitwa Karim na kumuua. Maisha yakasimama kwa familia hizi mbili katika kijiji hiki kidogo cha Misri. Familia ya Karim walitaka kulipiza kisasi, wakati ambapo familia ya Abdul-Rahman kwa hofu walijaribu kumlinda. Abdul-Rahman hakutaka mzunguko wa kulipiza kisasi uendelee. Aliomba ushauri kutoka kwa viongozi wa kijiji, na wakamshauri afanye tambiko la sanda ya kifo.

Abdul-Rahman alileta sanda yake mwenyewe nyeupe na kuweka kisu juu yake. Akatembea kwenda kukutana na familia ya Karim sokoni, wakati kijiji kizima kikiangalia. Abdul-Rahman alipiga magoti mbele ya Habibu, kaka wa marehemu, na kumkabidhi sanda na kisu. Alimwomba rehema na upatanisho.

Habibu aliweka kisu kuelekea shingoni mwa Abdul-Rahman. Viongozi wa kijiji walilete kondoo, na Habibu alipaswa kufanya uamuzi wake: rehema au kisasi? Alipoweka kisu kuelekea shingoni mwa Abdul-Rahman, matendo yake yalitangaza, “Sasa uko mikononi mwangu. Watu wote wanaliona hili; kila mtu anajua kuwa nina haki ya kukuua na uwezo wa kufanya hivyo. Lakini nachagua rehema na mapatano. Nitaukomesha uhasama huu wa damu.”

Akageuka kutoka kwa Abdul-Rahman na badala yake akamchinja yule kondoo. Baada ya mkurupuko wa uchungu, hasira, na haki kumezwa kabisa na mnyama yule, Habibu alimkumbatia Abdul-Rahman. Amani baina ya familia zile mbili ilirejeshwa. 

Kama wanadamu wanaweza kupata njia ya kuunganisha haki na rehema, ni hakika Mungu anaweza kufanya vivyo hivyo!  

Yesu Masihi: Rehema kutoka kwa Mungu

Ni wapi tunaweza kujifunza juu ya rehema ya Mungu? Ni jambo rahisi sana. Yumkini umewahi kusikia kwamba Yesu Masihi (Ambaye pia anajulikana kama Isa Al-Masih) anaitwa “Rehema” kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii ina maana kwamba Yeye ni mfano kamili wa rehema. Njia Yake—mafundisho Yake katika vitabu vya Injili, ambavyo pia vinaitwa Injil—hii ndiyo njia ya msamaha na upatanisho. 

Yesu Masihi anaweza kutimiza jukumu kama hilo la ajabu kwa sababu ni Yeye peke yake asiye na dhambi kabisa ambaye alitumwa na Mungu. Kila nabii na mjumbe mtakatifu alihitaji msamaha kwa ajili ya makosa yake, lakini haikuwa hivyo kwa Yesu Masihi. Alichukuliwa moja kwa moja kwenda mbinguni badala ya kusubiri Siku ya Kiyama kwa sababu hakuwahi kutenda kosa lolote—hata lililo dogo kabisa.

Kwa sababu hii anaitwa Rehema kutoka kwa Mungu. Alitupatia mfano wa rehema halisi na kufundisha jinsi ya kupokea rehema ya Mungu.

Je, ni jinsi gani Yesu Masihi anaweza kunisaidia?

Imeandikwa kwamba Yohana Mbatizaji (ajulikanaye pia kama Yahaya) alimwona Yesu Masihi katika umati, na kwa ufunuo (wahyi) kutoka kwa Mwenyezi Mungu, alipaza sauti “Tazama! Mwanakondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu!” (Injili, Yohana 1:29) Yesu Masihi ni kama kondoo yule aliyekuwa njia ya upatanisho kwa Abdul-Rahman. 

Tunapoadhibiwa kwa ajili ya makosa yetu, hii ndiyo haki. Lakini Yesu Masihi, ambaye hakuwa na dhambi kabisa, alijitolea kuwajibika kwa makosa yetu. Hakuna aliyemlazimisha. Kwa hiari Yake alikubali kufa ili kukidhi dai la haki. Alikuwa binadamu pekee ambaye hakuwa na hatia kabisa aliyewahi kuishi, na bado alikubali kutendewa kama yule kondoo aliyeelezwa katika kisa cha Abdul-Rahman. Hii ndiyo sababu, baada ya kuteseka kwa ajili yetu, Mungu alimwinua kwenda mbinguni. 

Huenda una mgogoro maishani mwako. Huenda wewe ni kama Fatuma, uliyetupwa na wale unaowapenda. Huenda umeumizwa na mtu fulani, au sifa yako imeharibiwa isivyo haki. Huenda wewe ni kama Abdul-Rahman, mwenye hatia na mwenye hofu ya kulipizwa kisasi.

Yesu Masihi anaweza kukusaidia. Unaweza tu kusali dua fupi kama hii:

Ee Bwana, kamwe siwezi kutoa fidia kwa ajili ya dhambi zangu. Lakini najua ulimtuma Yesu Masihi kama Rehema Yako kwetu. Tafadhali nisamehe kwa sababu ya kitendo chema alichotenda kwa jamii ya wanadamu wote. Nisaidie kuielewa njia ya Yesu Masihi ili niweze kupata rehema Zako maishani mwangu. Amina.

Kama ungependa kupata nakala yako binafsi ya Injili, tafadhali wasiliana nasi kupitia katika taarifa zilizo nyuma ya karatasi hii.

Copyright @ 2023 by Sharing Hope Publications. Kazi hii yaweza kuchapishwa na kusambazwa kwa watu wengine bure pasipo kuomba idhini kwa makusudi yasiyo ya kibiashara. 
Swahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.

Jisajili kwa ajili ya jarida letu

Kuwa wa kwanza kujua pale machapisho mapya yanapotoka

newsletter-cover