Usalama Dhidi ya Pepo Wachafu

Usalama Dhidi ya Pepo Wachafu

Muhtasari

Pepo wachafu wana nguvu, lakini hawana nguvu kama za Yesu Masihi. Kijitabu hiki kinaelezea jinsi Yesu alivyotoa pepo kutoka kwa watu waliokuwa wakiumwa na kuwasaidia kupata uponyaji. Anaweza kututendea vivyo hivyo leo. Kitabu chake kinatufundisha kila tunachohitaji kujua ili kuepukana na kunyanyaswa na kuteswa na pepo. Pia kinatufundisha jinsi ya kuepuka udanganyifu na ulaghai wa kishetani kabla ya kurejea Kwake

Pakua

Majini yapo kila mahali. Iwe unayaita roho, mizimu, mapepo, au majini, wanaweza kuogofya. Wafanya mazingaombwe, wachawi, na hirizi vimeenea, lakini je ni kweli vinaweza kutulinda?

Ningependa nishiriki nawe hatua tatu rahisi za kupata ulinzi dhidi ya pepo wachafu ili usiwaogope. 

Kinga Dhidi ya Pepo Wachafu

Mtu yule alikuwa uchi akilia kwa sauti ya juu. Alikuwa amepagawa na majini mengi, na hakukuwa na mtu aliyeweza kumsaidia. Watu wa kijijini mwake walikuwa wamejaribu kumfunga kwa minyororo, lakini aliivunja kwa nguvu kubwa kuliko ya kibinadamu naye alikimbia kwenda kuishi makaburini. Alitumia maisha yake kulia kwa namna ya kusikitisha sana na kujikatakata kwa mawe.

Hadi kufika kwa mtu aitwaye Yesu Kristo, ambaye pia anajulikana kama Isa al-Masih.

Mtu yule alikuwa ameteseka kiasi kwamba alipofungua kinywa chake kuomba msaada, majini walimlilia Yesu Kristo kwa nguvu kutaka asishughulike naye. Lakini Yesu hakuondoka. Alijua kilichokuwa kinafanyika. Pasipo hofu, Aliwaamuru majini wale kumtoka mtu yule.

“Usitupeleke shimoni!” majini waliomba. Waliomba waruhusiwe kuliingia kundi la nguruwe lililokuwa karibu pale. Yesu aliwaamuru wamtoke mtu yule na kuwaingia wale wanyama najisi. Mara ile, akili ikamrejea mtu yule, na kundi lote la nguruwe likakimbia na kuingia baharini.

Hatimaye, mtu yule alikuwa huru. Alishukuru sana! Lakini hiki si kisa pekee. Yesu Kristo alikuwa na nguvu kubwa mno juu ya pepo wachafu. Popote alipokwenda aliwaweka huru watu waliokuwa wamepagawa na majini. Pia aliwapa wafuasi wake mamlaka juu ya Ibilisi:

Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru. Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni (Injili, Luka 10:19, 20).

Tunapomfuata Yesu Kristo, tunaweza kuwa na usalama katika maisha haya na uhakika juu ya maisha yajayo! Hebu tutazame hatua tatu za kupata uhuru dhidi ya pepo wachafu.

Hatua ya 1: Dai Uwezo wa Jina la Yesu Kristo

Hatua ya kwanza ni kutafuta ulinzi wa Mungu katika jina la Yesu Kristo. Sisi wenyewe, hatuna nguvu. Lakini pale tunapolitangaza jina la Yesu Kristo katika maisha yetu, pepo wachafu wanaishiwa nguvu! Yesu alisema juu ya wafuasi wake: “Kwa jina langu watatoa pepo” (Injili, Marko 16:17).

Kama ukiamini kwa moyo wako wote kwamba Yesu Kristo atakuweka huru, atafanya hivyo! Wewe omba tu dua hii kwa Mungu, “Bwana, tafadhali niokoe na pepo wachafu katika jina la Yule uliyemtuma, Yesu Kristo!” 

Hatua ya 2: Tafuta Utakaso wa Ndani na Nje

Yesu Kristo alifundisha kwamba imetupasa kutompatia Ibilisi nafasi yoyote. Alisema, “kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu [Ibilisi], wala hana kitu kwangu” (Injili, Yohana 14:30). Ni lazima pia tusafishe maisha yetu kutokana na mivuto yote miovu. 

Je ni nini maana ya Ibilisi “hana kitu kwetu”? Yana maana kwamba hana kitu chochote katika mioyo au maskani yetu ambacho ni mali yake. Ni lazima tutupilie mbali talasimu na hirizi za kishirikina. Ni lazima tujiepushe na vitendo vyote viovu kama vile ponografia, dawa za kulevya, na pombe. Kama tumekuwa tukishiriki katika kaida za kuzungumza na wafu au kurusha laana, tunapaswa kuacha shughuli hizo mara moja. Hivyo, tunasafisha mazingira yetu ya nje dhidi ya mivuto ya kishetani. Kisha, imetupasa kumwomba Mungu atusamehe na kutusafisha kwa ndani.

Hatua ya 3: Jaza Maisha Yako na Nuru

Baada ya Yesu Kristo kukuokoa na nguvu za majini, mkaribishe apate kuwa mtawala wa maisha yako. Usiuache moyo wako mtupu. Yesu Kristo alisema,

Pepo mchafu, amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika, asipate. Halafu husema, “Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka.” Hata akija, aiona tupu, imefagiwa, na kupambwa. Mara huenda, akachukua pamoja naye pepo wengine saba walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kilicho kibaya (Injili, Mathayo 12:43–45).

Unapokuwa umesafishwa kutokana na majini, jaza maisha yako kwa nuru ya kitabu cha Yesu, Biblia. Yesu Kristo alikuja kama “nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani” (Injili, Yohana 12:46). Pata nakala ya kitabu cha Yesu na kukisoma kila siku ili nuru yake isukumizie mbali giza.

Usalama kwa Ajili ya Siku za Usoni

Tunaishi karibu na mwisho wa wakati ambapo roho wachafu wanafanya kazi kwa bidii kuliko wakati mwingine wowote. Yesu Kristo alitabiri kwamba kabla hajarudi, nguvu za giza zitafanya miujiza mingi ya bandia kujaribu kuwadanganya waumini. Kwa wengine, jini atajitokeza kwa namna ya kutisha kama mzuka; kwa wengine atajitokeza kama malaika au ndugu waliokufa. Ibilisi mwenyewe atajaribu kujifanya kuwa ni Yesu Kristo!

Lakini hupaswi kudanganywa na uongo huu. Kama ukimfuata Yesu Kristo, atakupa nguvu ya kumpinga Ibilisi. Rafiki mpendwa, haidhuru unapambana na nini kwa sasa, mruhusu Yesu akuweke huru!

Kama ungependa mfuasi wa Yesu Kristo akuombee ili upate kuwekwa huru kutokana na pepo wachafu, tafadhali wasiliana nasi katika taarifa iliyo nyuma ya karatasi hii.

Copyright @ 2023 by Sharing Hope Publications. Kazi hii yaweza kuchapishwa na kusambazwa kwa watu wengine bure pasipo kuomba idhini kwa makusudi yasiyo ya kibiashara. 
Swahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.

Jisajili kwa ajili ya jarida letu

Kuwa wa kwanza kujua pale machapisho mapya yanapotoka

newsletter-cover