Pasipo Hofu Hukumuni

Pasipo Hofu Hukumuni

Muhtasari

Kufikiria juu ya siku ya hukumu huamsha hofu mioyoni mwa watu wengi. Tunawezaje kuwa na uhakika kuwa tutapita salama katika siku ya kiyama? Mungu alisema kuwa atatupatia Mtetezi— Mtu wa kututetea katika hukumu kama wakili anavyokuwa mtetezi kwenye kesi katika mahakama za duniani. Kitini hiki kinatutambulisha kwa Mtetezi huyu na kutufundisha jinsi ya kuwa na uhakika kadiri tunavyotafakari juu ya hukumu inayokuja.

Aina

Kijitabu

Mchapishaji

Sharing Hope Publications

Inapatikana katika

39 Lugha

Kurasa

6

Pakua

Siku moja asubuhi niliondoka katika chumba changu cha hotelini kwenda kuhudhuria mkutano muhimu. Nilikuwa nimechelewa kwa hiyo niliendesha gari kwa kasi—kasi kubwa kuliko kikomo rasmi cha spidi. Nikiwa nusu ya safari yangu, askari polisi alinisimamisha na kuniambia imenipasa kwenda katika kituo cha polisi! Nilihisi wasiwasi sana na mnyonge kwa sababu nilijua kuwa nilikuwa na hatia. 

Baada ya askari polisi kufungua jalada la kesi dhidi yangu, nilipelekwa katika mahakama iliyokuwa karibu ili kusomewa mashtaka. Pale, nilitokea kukutana na rafiki yangu ambaye anafanya kazi kama mwanasheria. Alishangaa kuniona. Nilipoeleza yaliyonikuta, alisema, “Usiwe na wasiwasi. Nitaishughulikia kesi yako.” Nilifurahi sana. Rafiki yangu angekuwa ndiye wakili wangu!

Kwa kuwa rafiki yangu aliingia kunitetea, hakimu aliamua nitozwe faini ya kiwango cha chini. Niliondoka mahakamani nikimsifu Mungu.

Kwa kweli ni jambo la kuogofya kusimama mbele ya hakimu wa kidunia. Lakini hii si kitu ikilinganishwa na jinsi itakavyokuwa kusimama mbele za Mungu katika Siku ile kuu ya Kutoa Hesabu ya maisha yetu. Kama siku ile ingekuwa kesho, je ungekuwa tayari?

Kujiandaa kwa Ajili ya Hukumu

Baadhi ya watu huiitikia hukumu ijayo kwa mtazamo wa kizembe. Wanakunywa pombe, wanavuta sigara, wanacheza kamari, na kwenda kwenye vilabu vya usiku, na kuangalia video mbaya. Inawezekana kuwa wanajua kwamba vitu hivi vinaandikwa katika kitabu cha kumbukumbu lakini wamenaswa na madanganyo ya Shetani (anayejulikana pia kama Sheitwani). Hawajali.

Watu wengine huitikia kwa hofu iliyopitiliza. Hawathubutu kuacha kuomba hata mara moja. Wanafikiri mno juu ya mateso ya kaburini au moto wa kuzimu kiasi kwamba wanasahau upendo na huruma za Mungu. 

Lakini kama ambavyo nilikuwa na wakili pale mahakamani, Mungu ametupatia wakili atakayetusaidia kupita hukumuni. Hutakuwa na haja ya kuwa peke yako!

Je, Wakili wetu ni nani?

Wazo la Wakili si jipya. Kila mwaka maelfu ya mahujaji hutembelea madhabahu kule Afrika ya Kaskazini, Mashariki ya Kati, na Asia. Watu wengi hufanya sala katika makaburi ya viongozi mashuhuri, wakiamini kuwa watakuwa watetezi wao. 

Ni jambo jema kuwaheshimu hao viongozi wakuu, lakini kuwaabudu au kuomba watuombee ni haramu kabisa. Wao ni wafu na hawawezi kufanya lolote kwa ajili yako. Hata manabii wako makaburini mwao, wakiingoja Siku ya Ufufuo.

Ingawa ni haramu kuwaomba wafu kutuombea, wazo lenyewe la kuombewa ni sahihi. Lakini je, ni maombezi ya nani yanayokubalika mbele za Mungu? Ni lazima awe yule ambaye 

  1. Yu hai (kwa sababu wafu hawawezi kuzungumza kwa niaba yetu). 

  2. Asiye na dhambi (kwa sababu anayetiwa hatiani na sheria hawezi kuwa wakili wa watu wengine).

Ni nani aliye na sifa hizi? Si mwingine bali ni mpendwa Yesu Kristo, ajulikanaye pia kama Isa al-Masih, Yeye aliye hai mbinguni na msafi pasipo waa lolote. 

Hebu litafakari hili—Je kuna mtu mwingine yeyote anayeweza kudai kutokuwa na dhambi? Adamu alikula tunda lililokatazwa; Nuhu alilewa kwa mvinyo; Ibrahimu alisema uongo; Musa aliua mtu; Daudi aliiba mke wa mtu mwingine. Hutapata nabii hata mmoja ambaye hakuwahi kufanya kosa hata moja au ambaye hakuwahi kuomba msamaha.

Lakini Yesu Kristo kamwe hakutenda dhambi yoyote. Yeye Mwenyewe alisema, “Naye aliyenipeleka yu pamoja nami . . . . kwa sababu nafanya sikuzote yale yampendezayo” (kutoka katika Injili, Yohana 8:29). 

Kuikabili Hukumu kwa Amani

Yesu Kristo Yu hai mbinguni na hana dhambi kabisa. Yuko tayari kututetea mimi pamoja nawe. Naye atarejea punde.

Kama anakuja mara ya pili, ina maana kwamba Yesu Kristo ndiye nabii wa mwisho. Ndio, na zaidi ya nabii—Yeye ni Wakili, Bwana, na Amani yetu katika Siku ile ya kiyama. Alituambia, “Amin, amin, nawaambia, Mtu akilishika neno langu, hataona mauti milele” (Injili, Yohana 8:51). 

Yesu si mfu; Yu hai! Naye anaijenga jamii ya watu wake duniani hata sasa. Nyakati zingine anawaita watu kujiunga na jamii ya watu wake kwa njia ya kuonekana katika ndoto kama mwanadamu aliyevalia mavazi meupe au kwa kufanya miujiza tunapomwomba Mungu kwa jina lake. 

Je unataka kuwa na amani katika Siku ile ya Kiyama? Kiri kuwa na imani kwa Yesu Kristo. Kwa nini tuweke imani yetu kwa watu waliokufa na ambao hawajui nini kitawapata katika Siku ile ya kiyama? Yesu ana hakika na nafasi yake mbinguni. Kama yule mwanasheria rafiki yangu katika chumba cha mahakama, atatusaidia.

Inawezekana ukawa unajiuliza iwapo kitu kizuri kiasi hicho kinaweza kuwa kweli. Yesu Kristo alisema, “Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya” (Injili, Yohana14:14). Hebu fanya jaribio ili upate kuthibitisha kama ninachokuambia ni kweli. Kama Yesu ana uweza wa kutosha kukabiliana na dharura za maisha sasa hivi, basi ni hakika anaweza kuaminika kuwa wakili wetu. Mwombe Mungu kwa jina la Yesu kwa moyo wa dhati na uone kitakachotokea. Unaweza kuomba:

Ee Bwana, ningependa kujua kama kweli Yesu ndiye hasa uliyemteua kuwa wakili wetu katika hukumu. Kama ni kweli tafadhali jibu ombi langu (ingiza hitaji lako hapa). Ninaomba hili katika jina la Yesu Kristo. Amina.

Kama ungependa kujua zaidi juu ya jinsi ya kumfuata Yesu Kristo, wasiliana nasi katika taarifa iliyo nyuma ya karatasi hii.

Copyright @ 2023 by Sharing Hope Publications. Kazi hii yaweza kuchapishwa na kusambazwa kwa watu wengine bure pasipo kuomba idhini kwa makusudi yasiyo ya kibiashara. Swahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.

Jisajili kwa ajili ya jarida letu

Kuwa wa kwanza kujua pale machapisho mapya yanapotoka

newsletter-cover